Deuteronomy 8

Usimsahau Bwana

1 aUwe mwangalifu kufuata kila agizo ninalokupa wewe leo, ili mweze kuishi, kuongezeka na mweze kuingia mkamiliki nchi ambayo Bwana aliahidi kwa kiapo kwa baba zenu. 2 bKumbuka jinsi Bwana Mwenyezi Mungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. 3 cAlikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana. 4 dNguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini. 5 eMjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo Bwana Mwenyezi Mungu wako atawaadibisha ninyi.

6 fShikeni maagizo ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu mtembee katika njia zake na kumheshimu. 7 gKwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima; 8 hnchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali; 9 inchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima.

10 jWakati mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Bwana Mwenyezi Mungu wenu kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa. 11 kJihadharini msimsahau Bwana Mwenyezi Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo. 12 lAngalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo, 13na wakati makundi yenu ya ng’ombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa, 14 mbasi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Bwana Mwenyezi Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 nAliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. 16 oAliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekesha na kuwajaribu ninyi ili mwishoni apate kuwatendea mema. 17 pMnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 qLakini kumbukeni Bwana Mwenyezi Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

19 rIkiwa mtamsahau Bwana Mwenyezi Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa. 20 sKama mataifa Bwana aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii Bwana Mwenyezi Mungu wenu.
Copyright information for SwhKC